1 Wakorintho 10
Swahili NT
1Ndugu, nataka mjue kwamba babu zetu wote walikuwa chini ya ulinzi wa lile wingu, na kwamba wote walivuka salama ile bahari. 2Wote walibatizwa katika umoja na Mose kwa lile wingu na ile bahari. 3Wote walikula chakula kilekile cha kiroho, 4wakanywa pia kinywaji kilekile cha kiroho, maana walikunywa kutoka ule mwamba wa kiroho uliowafuata; mwamba huo ulikuwa Kristo mwenyewe. 5Hata hivyo, wengi wao hawakumpendeza Mungu, na maiti zao zilisambazwa jangwani.

6Sasa, mambo hayo yote ni mfano tu kwetu; yanatuonya sisi tusitamani ubaya kama wao walivyotamani. 7Msiwe waabudu sanamu kama baadhi yao walivyokuwa; kama yasemavyo Maandiko: "Watu waliketi kula na kunywa, wakasimama kucheza." 8Wala tusizini kama baadhi yao walivyozini, wakaangamia siku moja watu ishirini na tatu elfu. 9Tusimjaribu Bwana kama baadhi yao walivyomjaribu, wakauawa na nyoka. 10Wala msinung'unike kama baadhi yao walivyonung'unika, wakaangamizwa na Mwangamizi! 11Basi, mambo hayo yaliyowapata wao ni kielelezo kwa wengine, na yaliandikwa ili kutuonya sisi, ambao mwisho wa nyakati unatukabili. 12Anayedhani amesimama imara ajihadhari asianguke. 13Majaribu mliyokwisha pata ni ya kawaida kwa binadamu. Mungu ni mwaminifu, naye hataruhusu mjaribiwe kupita nguvu zenu, ila pamoja na majaribu, yeye atawapeni pia nguvu ya kustahimili na njia ya kutoka humo salama.

14Kwa hiyo, wapenzi wangu, epeni ibada za sanamu. 15Naongea nanyi, watu wenye busara; jiamulieni wenyewe hayo nisemayo. 16Tunapomshukuru Mungu kwa kikombe kile cha baraka, je, huwa hatushiriki damu ya Kristo? Na tunapoumega mkate, je, huwa hatushiriki mwili wa Kristo? 17Kwa kuwa mkate huo ni mmoja, sisi, ingawa ni wengi, tu mwili mmoja; maana sote twashiriki mkate huohuo. 18Chukueni, kwa mfano, Wayahudi wenyewe: kwao, wenye kula vilivyotambikiwa madhabahuni waliungana na hiyo madhabahu. 19Nataka kusema nini, basi? Kwamba chakula kilichotambikiwa sanamu ni kitu zaidi ya chakula? Na hizo sanamu, je, ni kitu kweli zaidi ya sanamu? 20Hata kidogo! Ninachosema ni kwamba tambiko wanazotoa watu wasiomjua Mungu wanawatolea pepo, sio Mungu. Sipendi kamwe ninyi muwe na ushirika na pepo. 21Hamwezi kunywa kikombe cha Bwana na kikombe cha pepo; hamwezi kushiriki katika meza ya Bwana na katika meza ya pepo. 22Au je, tunataka kumfanya Bwana awe na wivu? Mnadhani tuna nguvu zaidi kuliko yeye?

23Vitu vyote ni halali, lakini si vyote vinafaa. Vitu vyote ni halali lakini si vyote vinajenga. 24Mtu asitafute faida yake mwenyewe, ila faida ya mwenzake. 25Kuleni chochote kile kiuzwacho sokoni bila ya kuulizauliza kwa sababu ya dhamiri zenu; 26maana Maandiko yasema: "Dunia na vyote vilivyomo ni mali ya Bwana." 27Kama mtu ambaye si muumini akiwaalikeni nanyi mkakubali kwenda, basi, kuleni vyote atakavyowaandalieni bila kuulizauliza kwa sababu ya dhamiri zenu. 28Lakini mtu akiwaambieni: "Chakula hiki kimetambikiwa sanamu," basi, kwa ajili ya huyo aliyewaambieni hivyo na kwa ajili ya dhamiri, msile. 29Nasema, "kwa ajili ya dhamiri," si dhamiri yenu, bali dhamiri yake huyo aliyewaambieni. Mtaniuliza: "Kwa nini uhuru wangu utegemee dhamiri ya mtu mwingine? 30Ikiwa mimi nashiriki chakula hicho huku namshukuru Mungu, kwa nini nilaumiwe kwa chakula ambacho kwa ajili yake nimemshukuru Mungu?"

31Basi, chochote mfanyacho iwe ni kula au kunywa, fanyeni yote kwa ajili ya utukufu wa Mungu. 32Msiwe kikwazo kwa Wayahudi au kwa Wagiriki au kwa kanisa la Mungu. 33Muwe kama mimi; najaribu kuwapendeza wote kwa kila njia, bila kutafuta faida yangu mwenyewe ila faida ya wote, wapate kuokolewa.



Public Domain Swahili New Testament -- PLEASE MAKE COPIES FOR YOUR FRIENDS, NO ROYALTY DUE.

Bible Hub

1 Corinthians 9
Top of Page
Top of Page