1 Petro 3
Swahili NT
1Nanyi wake, jiwekeni chini ya mamlaka ya waume zenu, ili kama wako waume wowote wasioamini neno la Mungu, wapate kuamini kwa kuuona mwenendo wenu. Haitakuwa lazima kwenu kusema neno, 2kwani wataona jinsi mwenendo wenu ulivyo safi na wa kumcha Mungu. 3Katika kujipamba kwenu msitegemee mambo ya njenje, kama vile mitindo ya kusuka nywele, kujivalia vitu vya dhahabu na nguo maridadi. 4Bali, uzuri wenu unapaswa kutokana na hali ya ndani ya utu wa kweli, uzuri usioharibika wa wema na utulivu wa roho, ambao ni wa thamani kubwa mbele ya Mungu. 5Ndivyo walivyojipamba hapo kale wanawake waadilifu waliomtumainia Mungu; walijiweka chini ya mamlaka ya waume zao. 6Sara kwa mfano alimtii Abrahamu na kumwita yeye bwana. Ninyi mmekuwa sasa binti zake kama mkitenda mema bila kuogopa tisho lolote.

7Kadhalika nanyi waume, katika kuishi na wake zenu mnapaswa kutambua kwamba wao ni dhaifu na hivyo muwatendee kwa heshima; maana nao pia watapokea pamoja nanyi zawadi ya uzima anayowapeni Mungu. Hapo ndipo sala zenu hazitakataliwa.

8Mwisho nasema hivi: mnapaswa kuwa na moyo mmoja, na fikira moja; mnapaswa kupendana kidugu, kuwa wapole na wanyenyekevu ninyi kwa ninyi. 9Msiwalipe watu ovu kwa ovu, au tusi kwa tusi; bali watakieni baraka, maana ninyi mliitwa na Mungu mpate kupokea baraka.

10Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: "Anayetaka kufurahia maisha, na kuona siku za fanaka, anapaswa kuacha kusema mabaya na kuacha kusema uongo.

11Na ajiepushe na uovu, atende mema, atafute amani na kuizingatia.

12Maana Bwana huwatazama kwa wema waadilifu na kuzisikiliza sala zao. Lakini huwapa kisogo watu watendao maovu."

13Ni nani atakayeweza kuwadhuru ninyi kama mkizingatia kutenda mema? 14Lakini, hata kama itawapasa kuteseka kwa sababu ya kutenda mema, basi, mna heri. Msimwogope mtu yeyote, wala msikubali kutiwa katika wasiwasi. 15Lakini mtukuzeni Kristo kama Bwana mioyoni mwenu. Muwe tayari kumjibu yeyote atakayewaulizeni juu ya matumaini yaliyo ndani yenu, 16lakini fanyeni hivyo kwa upole na heshima. Muwe na dhamiri njema, kusudi mnapotukanwa, wale wanaosema ubaya juu ya mwenendo wenu mwema kama Wakristo, waone aibu. 17Maana ni afadhali kuteseka kwa sababu ya kutenda mema, kama Mungu akipenda, kuliko kuteseka kwa sababu ya kutenda uovu. 18Kwa maana Kristo mwenyewe alikufa kwa ajili ya dhambi zenu; alikufa mara moja tu na ikatosha, mtu mwema kwa ajili ya waovu, ili awapeleke ninyi kwa Mungu. Aliuawa kimwili lakini akafanywa hai kiroho; 19na kwa maisha yake ya kiroho alikwenda kuwahubiria wale roho waliokuwa kifungoni. 20Hao ndio wale waliokataa kumtii Mungu alipowangoja kwa saburi wakati Noa alipokuwa anatayarisha ile safina. Ndani ya chombo hicho ni watu wachache tu, yaani watu wanane, waliookolewa majini, 21ambayo yalikuwa mfano wa ubatizo unaowaokoa ninyi sasa. Ubatizo si shauri la kuondoa uchafu mwilini, bali ni ahadi kwa Mungu inayofanyika katika dhamiri njema. Huwaokoeni kwa njia ya ufufuo wa Yesu Kristo, 22ambaye alikwenda mbinguni na sasa amekaa upande wa kulia wa Mungu, anatawala juu ya malaika, wakuu na wenye enzi.



Public Domain Swahili New Testament -- PLEASE MAKE COPIES FOR YOUR FRIENDS, NO ROYALTY DUE.

Bible Hub

1 Peter 2
Top of Page
Top of Page