Matayo 14
Swahili NT
1Wakati huo, mtawala Herode alisikia sifa za Yesu. 2Basi, akawaambia watumishi wake, "Mtu huyu ni Yohane mbatizaji, amefufuka kutoka wafu; ndiyo maana nguvu za miujiza zinafanya kazi ndani yake."

3Herode ndiye aliyekuwa amemtia Yohane nguvuni, akamfunga minyororo na kumtia gerezani kwa sababu ya Herodia, mke wa Filipo, ndugu yake. Sababu hasa ni 4kwamba alikuwa amemwambia Herode, "Si halali kwako kuishi na huyo mwanamke!" 5Herode alitaka kumwua Yohane, lakini aliogopa watu kwa sababu kwao Yohane alikuwa nabii.

6Katika sherehe za sikukuu ya kuzaliwa kwake Herode, binti ya Herodia alicheza mbele ya wageni. Herode alifurahiwa, 7hata akaahidi kwa kiapo kumpa huyo msichana chochote atakachoomba. 8Naye, huku akichochewa na mama yake, akaomba, "Nipe papahapa katika sinia kichwa cha Yohane mbatizaji." 9Mfalme alihuzunika, lakini kwa sababu ya kile kiapo chake na kwa sababu ya wale wageni karamuni, akaamuru apewe. 10Basi, Herode akatuma mtu gerezani amkate kichwa Yohane. 11Kichwa chake kikaletwa katika sinia, wakampa yule msichana, naye akampelekea mama yake. 12Wanafunzi wa Yohane wakaja, wakauchukua mwili wake, wakauzika. Kisha wakaenda kumpasha habari Yesu.

13Yesu alipopata habari hiyo, aliondoka mahali pale kwa mashua, akaenda mahali pa faragha peke yake. Lakini watu walipata habari, wakamfuata kwa miguu toka mijini. 14Basi, aliposhuka pwani, aliona umati mkubwa wa watu, akawaonea huruma, akawaponya wagonjwa wao.

15Kulipokuwa jioni, wanafunzi wake walimwendea wakamwambia, "Mahali hapa ni nyikani, na saa zimepita. Basi, uwaage watu ili waende vijijini wakajinunulie chakula." 16Yesu akawaambia, "Si lazima waende, wapeni ninyi chakula." 17Lakini wao wakamwambia, "Tunayo mikate mitano tu na samaki wawili." 18Yesu akawaambia, "Nileteeni hapa." 19Akawaamuru watu waketi katika nyasi. Kisha akaitwaa ile mikate mitano na wale samaki wawili, akatazama juu mbinguni, akamshukuru Mungu. Halafu akaimega hiyo mikate, akawapa wanafunzi wake, nao wakawapa watu. 20Watu wote wakala, wakashiba. Kisha wanafunzi wakakusanya mabaki, wakajaza vikapu kumi na viwili. 21Jumla ya waliokula ilikuwa wanaume wapatao elfu tano, bila kuhesabu wanawake na watoto.

22Mara, Yesu akawaamuru wanafunzi wake wapande mashua, wamtangulie ng'ambo ya ziwa wakati yeye anawaaga watu. 23Baada ya kuwaaga, alipanda mlimani peke yake kusali. Ilipokuwa jioni, yeye alikuwa huko peke yake, 24na wakati huo ile mashua ilikwishafika karibu katikati ya ziwa, lakini ilikuwa inakwenda mrama kwa sababu upepo ulikuwa unaipinga. 25Usiku, karibu na mapambazuko, Yesu aliwaendea wanafunzi akitembea juu ya maji. 26Wanafunzi wake walipomwona akitembea juu ya maji waliingiwa na hofu, wakasema, "Ni mzimu!" Wakapiga kelele kwa hofu. 27Mara, Yesu akasema nao, "Tulieni, ni mimi. Msiogope!"

28Petro akamwambia, "Bwana, ikiwa ni wewe kweli, amuru nitembee juu ya maji nije kwako." 29Yesu akasema, "Haya, njoo." Basi, Petro akashuka kutoka ile mashua, akatembea juu ya maji, akamwendea Yesu. 30Lakini alipouona ule upepo, aliogopa, akaanza kuzama; akalia kwa sauti, "Bwana, niokoe!" 31Hapo, Yesu akaunyosha mkono wake, akamshika na kumwambia, "Ewe mwenye imani haba! Kwa nini uliona shaka?" 32Basi, wakapanda mashuani, na upepo ukatulia. 33Wote waliokuwa ndani ya mashua walimsujudia, wakasema, "Hakika wewe ni Mwana wa Mungu."

34Walivuka ziwa, wakafika nchi ya Genesareti. 35Watu wa huko walipomtambua, wakaeneza habari pote katika sehemu hizo. Basi, wakamletea Yesu wagonjwa wote, 36wakamwomba awaruhusu waguse tu pindo la vazi lake; wote waliomgusa walipona.



Public Domain Swahili New Testament -- PLEASE MAKE COPIES FOR YOUR FRIENDS, NO ROYALTY DUE.

Bible Hub

Matthew 13
Top of Page
Top of Page