Matayo 15
Swahili NT
1Kisha Mafarisayo na walimu wa Sheria wakafika kutoka Yerusalemu, wakamwendea Yesu, wakamwuliza, 2Kwa nini wanafunzi wako hawajali mapokeo tuliyopokea kutoka kwa wazee wetu? Hawanawi mikono yao kama ipasavyo kabla ya kula! 3Yesu akawajibu, "Kwa nini nanyi mnapendelea mapokeo yenu wenyewe na hamuijali Sheria ya Mungu? 4Mungu amesema: Waheshimu baba yako na mama yako, na Anayemkashifu baba yake au mama yake, lazima auawe. 5Lakini ninyi mwafundisha ati mtu akiwa na kitu ambacho angeweza kuwasaidia nacho baba au mama yake, lakini akasema: Kitu hiki nimemtolea Mungu, 6basi, hapaswi tena kumheshimu baba yake! Ndivyo mnavyodharau neno la Mungu kwa kufuata mafundisho yenu wenyewe. 7Enyi wanafiki! Isaya alitabiri sawa kabisa juu yenu:

8Watu hawa, asema Mungu, huniheshimu kwa maneno tu, lakini mioyoni mwao wako mbali nami.

9Kuniabudu kwao hakufai, maana mambo wanayofundisha ni maagizo ya kibinadamu tu."

10Yesu aliuita ule umati wa watu, akawaambia, "Sikilizeni na muelewe! 11Kitu kinachomtia mtu najisi si kile kiingiacho kinywani, bali kile kitokacho kinywani. Hicho ndicho kimtiacho mtu najisi."

12Kisha wanafunzi wakamwendea, wakamwambia, "Je, unajua kwamba Mafarisayo walichukizwa waliposikia maneno yako?" 13Lakini yeye akawajibu, "Kila mmea ambao Baba yangu aliye mbinguni hakuupanda, utang'olewa. 14Waacheni wenyewe! Wao ni vipofu, viongozi wa vipofu; na kipofu akimwongoza kipofu, wote wawili hutumbukia shimoni."

15Petro akadakia, "Tufafanulie huo mfano." 16Yesu akasema, "Hata nyinyi hamwelewi? 17Je, hamwelewi kwamba kila kinachoingia kinywani huenda tumboni na baadaye hutupwa nje chooni? 18Lakini yale yatokayo kinywani hutoka moyoni, na hayo ndiyo yanayomtia mtu najisi. 19Maana moyoni hutoka mawazo maovu yanayosababisha uuaji, uzinzi, uasherati, wizi, ushahidi wa uongo na kashfa. 20Hayo ndiyo yanayomtia mtu najisi. Lakini kula chakula bila kunawa mikono hakumtii mtu najisi."

21Yesu aliondoka mahali hapo akaenda kukaa katika sehemu za Tiro na Sidoni. 22Basi, mama mmoja Mkaanani wa nchi hiyo alimjia, akapaaza sauti: "Mheshimiwa, Mwana wa Daudi, nionee huruma! Binti yangu anasumbuliwa na pepo." 23Lakini Yesu hakumjibu neno. Basi, wanafunzi wake wakamwendea, wakamwambia, "Mwambie aende zake kwa maana anatufuatafuata akipiga kelele." 24Yesu akajibu, "Sikutumwa ila kwa watu wa Israeli waliopotea kama kondoo." 25Hapo huyo mama akaja, akapiga magoti mbele yake, akasema, "Mheshimiwa, nisaidie." 26Yesu akamjibu, "Si sawa kuchukua chakula cha watoto na kuwatupia mbwa." 27Huyo mama akajibu, "Ni kweli, Mheshimiwa; lakini hata mbwa hula makombo yanayoanguka kutoka meza ya bwana wao." 28Hapo Yesu akamjibu, "Mama, imani yako ni kubwa; basi, ufanyiwe kama unavyotaka." Yule binti yake akapona tangu saa hiyo wakati huohuo.

29Yesu alitoka hapo akaenda kando ya ziwa Galilaya, akapanda mlimani, akaketi. 30Watu wengi sana wakamjia wakiwaleta vilema, vipofu, viwete, bubu na wengine wengi waliokuwa wagonjwa, wakawaweka mbele ya miguu yake, naye Yesu akawaponya. 31Umati ule wa watu ulishangaa sana ulipoona bubu wakiongea, waliokuwa wamelemaa wamepona, viwete wakitembea na vipofu wakiona; wakamsifu Mungu wa Israeli.

32Basi, Yesu aliwaita wanafunzi wake, akasema, "Nawaonea watu hawa huruma kwa sababu kwa siku tatu wamekuwa nami, wala hawana chakula. Sipendi kuwaacha waende bila kula wasije wakazimia njiani." 33Wanafunzi wakamwambia, "Hapa tuko nyikani; tutapata wapi chakula cha kuwatosha watu wengi hivi?" 34Yesu akawauliza, "Mnayo mikate mingapi?" Wakamjibu, "Saba na visamaki vichache." 35Basi, Yesu akawaamuru watu wakae chini. 36Akaitwaa ile mikate saba na vile visamaki, akamshukuru Mungu, akavimega, akawapa wanafunzi, nao wakawagawia watu. 37Wote wakala, wakashiba. Kisha wakakusanya makombo, wakajaza vikapu saba. 38Hao waliokula walikuwa wanaume elfu nne, bila kuhesabu wanawake na watoto.

39Basi, Yesu akawaaga watu, akapanda mashua, akaenda katika eneo la Magadani.



Public Domain Swahili New Testament -- PLEASE MAKE COPIES FOR YOUR FRIENDS, NO ROYALTY DUE.

Bible Hub

Matthew 14
Top of Page
Top of Page