Ufunua was Yohana 1
Swahili NT
1Hizi ni habari za mambo ambayo yalifunuliwa na Yesu Kristo. Mungu alimpa Kristo ufunuo huu ili awaonyeshe watumishi wake mambo ambayo yanapaswa kutukia karibuni. Kristo alimtuma malaika wake amjulishe Yohane, mtumishi wake, mambo hayo, 2naye Yohane, ameyasema yote aliyoyaona. Na hii ndio taarifa yake kuhusu ujumbe wa Mungu na ukweli uliofunuliwa na Yesu Kristo. 3Heri yake mtu anayesoma kitabu hiki; heri yao wale wanaosikiliza maneno ya ujumbe huu wa kinabii na kushika yaliyoandikwa humu, maana wakati umekaribia ambapo mambo haya yatatukia.

4Mimi Yohane nayaandikia makanisa yaliyoko mkoani Asia. Nawatakieni neema na amani kutoka kwake yeye aliyeko, aliyekuwako na anayekuja; na kutoka kwa roho saba walio mbele ya kiti chake cha enzi, 5na kutoka kwa Yesu Kristo, shahidi mwaminifu, wa kwanza kufufuliwa kutoka wafu, na ambaye ni mtawala wa wafalme wa dunia. Yeye anatupenda, na kwa damu yake ametufungua kutoka vifungo vya dhambi zetu, 6akatufanya sisi kuwa ufalme wa makuhani, tumtumikie Mungu, Baba yake. Kwake Yesu Kristo uwe utukufu na nguvu, milele na milele! Amina. 7Tazama! Anakuja katika mawingu! Kila mtu atamwona, hata wale waliomchoma. Makabila yote duniani yataomboleza juu yake. Naam! Amina.

8Mimi ni Alfa na Omega, asema Bwana Mungu Mwenye Uwezo, aliyeko, aliyekuwako na anayekuja.

9Mimi ni Yohane, ndugu yenu; na kwa kuungana na Kristo nashiriki pamoja nanyi katika kustahimili mateso yanayowapata wale walio wa Utawala wake. Mimi nilikuwa kisiwani Patmo kwa sababu ya kuhubiri ujumbe wa Mungu na ukweli wa Yesu. 10Basi, wakati mmoja, siku ya Bwana, nilikumbwa na Roho, nikasikia nyuma yangu sauti kubwa kama sauti ya tarumbeta. 11Nayo ilisema, "Andika katika kitabu yote unayoyaona, ukipeleke kwa makanisa haya saba: Efeso, Smurna, Pergamoni, Thuatira, Sarde, Filadelfia na Laodikea."

12Basi, nikageuka nimwone huyo aliyesema nami, nikaona vinara vya taa saba vya dhahabu, 13na katikati yake kulikuwa na kitu kama mtu, naye alikuwa amevaa kanzu ndefu na ukanda wa dhahabu kifuani. 14Nywele zake zilikuwa nyeupe kama pamba safi, kama theluji; macho yake yalimetameta kama moto; 15miguu yake iling'aa kama shaba iliyosafishwa katika tanuru ya moto na kusuguliwa, na sauti yake ilikuwa, kama sauti ya poromoko la maji. 16Katika mkono wake wa kulia, alikuwa na nyota saba, na kinywani mwake mlitoka upanga wenye makali kuwili. Uso wake uling'aa kama jua kali.

17Basi, nilipomwona tu, nilianguka mbele ya miguu yake kama maiti. Lakini yeye akaweka mkono wake wa kulia juu yangu, akasema, "Usiogope! Mimi ni wa kwanza na wa mwisho. 18Mimi ni yeye aliye hai! Nilikuwa nimekufa, lakini, tazama, sasa ni mzima milele na milele. Ninazo funguo za kifo na Kuzimu. 19Basi, sasa andika mambo haya unayoyaona, mambo yanayotukia sasa na yale yatakayotukia baadaye. 20Siri ya nyota zile saba ulizoziona katika mkono wangu wa kulia, na siri ya vile vinara saba vya taa hii: zile nyota saba ni malaika wa makanisa; na vile vinara saba vya taa ni makanisa saba.



Public Domain Swahili New Testament -- PLEASE MAKE COPIES FOR YOUR FRIENDS, NO ROYALTY DUE.

Bible Hub

Jude 1
Top of Page
Top of Page