Ufunua was Yohana 9
Swahili NT
1Kisha malaika wa tano akapiga tarumbeta yake. Nami nikaona nyota iliyokuwa imeanguka juu ya nchi kutoka mbinguni. Nayo ikapewa ufunguo wa shimo la Kuzimu. 2Basi, nyota hiyo ikafungua shimo la Kuzimu, kukatoka moshi wa tanuru kubwa. Jua na anga vikatiwa giza kwa moshi huo wa Kuzimu. 3Nzige wakatoka katika moshi huo, wakaingia duniani wakapewa nguvu kama ya ng'e. 4Wakaamrishwa wasiharibu nyasi za nchi wala majani wala miti yoyote, bali wawaharibu wale tu ambao hawakupigwa mhuri wa Mungu katika paji la uso. 5Nzige hao hawakuruhusiwa kuwaua watu, ila kuwatesa tu kwa muda wa miezi mitano. Maumivu watakayosababisha ni kama maumivu yanayompata mtu wakati anapoumwa na ng'e. 6Muda huo watu watatafuta kifo lakini hawatakipata; watatamani kufa lakini kifo kitawakimbia.

7Kwa kuonekana, nzige hao walikuwa kama farasi waliowekwa tayari kwa vita. Juu ya vichwa vyao walikuwa na taji zilizo kama za dhahabu, na nyuso zao zilikuwa kama za binadamu. 8Nywele zao zilikuwa kama nywele za wanawake, na meno yao yalikuwa kama meno ya simba. 9Vifua vyao vilikuwa vimefunikwa kitu kama ngao ya chuma. Sauti ya mabawa yao ilikuwa kama sauti ya msafara wa magari ya farasi wengi wanaokimbilia vitani. 10Walikuwa na mikia na miiba kama ng'e, na kwa mikia hiyo, walikuwa na nguvu ya kuwadhuru watu kwa muda wa miezi mitano. 11Tena wanaye mfalme anayewatawala, naye ndiye malaika wa kuzimu; jina lake kwa Kiebrania ni Abadoni, na kwa Kigiriki ni Apolioni, yaani mwangamizi.

12Maafa ya kwanza yamepita; bado mengine mawili yanafuata.

13Kisha malaika wa sita akapiga tarumbeta yake. Nami nikasikia sauti moja kutoka katika pembe nne za madhabahu ya dhahabu iliyokuwa mbele ya Mungu. 14Sauti hiyo ikamwambia huyo malaika wa sita mwenye tarumbeta, "Wafungulie malaika wanne waliofungwa kwenye mto mkubwa Eufrate!" 15Naye akawafungulia malaika hao wanne ambao walikuwa wametayarishwa kwa ajili ya saa hiyo ya siku ya mwezi huo, wa mwaka huohuo, kuua theluthi moja ya wanaadamu. 16Nilisikia idadi ya majeshi wapanda farasi ilikuwa milioni mia mbili. 17Hivi ndivyo nilivyowaona hao farasi na wapanda farasi katika hiyo njozi: Walikuwa na ngao vifuani zilizokuwa moto mtupu, zenye rangi ya samawati na njano kama kiberiti. Vichwa vya hao farasi vilikuwa kama vya simba; na moto, moshi, na kiberiti vilikuwa vinatoka kinywani mwao. 18Theluthi moja ya wanaadamu waliuawa kwa mabaa hayo matatu yaani, moto, moshi na kiberiti, yaliyokuwa yanatoka katika vinywa vyao; 19maana nguvu ya farasi hao ilikuwa vinywani mwao na katika mikia yao. Mikia yao ilikuwa na vichwa kama nyoka, na waliitumia hiyo kuwadhuru watu.

20Wanaadamu wengine waliobaki ambao hawakuuawa na mabaa hayo, hawakugeuka na kuviacha vitu walivyokuwa wametengeneza kwa mikono yao wenyewe; bali wakaendelea kuabudu pepo, sanamu za dhahabu, fedha, shaba, mawe na miti, vitu ambavyo haviwezi kuona, kusikia wala kutembea. 21Wala hawakutubu na kuacha kufanya mauaji, uchawi, uzinzi, na wizi.



Public Domain Swahili New Testament -- PLEASE MAKE COPIES FOR YOUR FRIENDS, NO ROYALTY DUE.

Bible Hub

Revelation 8
Top of Page
Top of Page